Tuesday, 22 April 2025

TIKA KUTOA MASHINE ZA KUONGEZA THAMANI KWA MAHINDI KWA VIKUNDI 55 JIMBO LA PERAMIHO


Takriban vikundi 55 vya maendeleo kutoka kata 18 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, vinatarajiwa kunufaika na mashine za kuongeza thamani ya zao la mahindi zitakazotolewa na Shirika la Kiserikali la Uturuki (TIKA).

Katika ufadhili huo, vikundi 23 vitapokea mashine za kusaga na kukoboa mahindi, huku vikundi 32 vikipewa mashine za kupukuchua mahindi.

Filiz Sahinci, Mratibu wa Programu za TIKA nchini Tanzania, akizungumza katika ziara ya kutembelea vikundi hivyo, amesema moja ya malengo ya shirika hilo ni kuwawezesha wananchi wa hali ya chini kiuchumi kwa kuwasaidia katika changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kiuchumi hasa wakiwa wamelilenga kundi la wanawake, amesema kuwa “Mwanamke akiwa na nguvu ya kiuchumi, jamii nzima itakuwa na uchumi imara.”




Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Peramiho ambaye pia ni Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amelipongeza shirika la TIKA kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.

Mhe. Mhagama ametoatoa wito kwa wananchi wanaonufaika na mashine hizo kuendelea kujikita katika uzalishaji wa mazao na kuzitumia vyema fursa walizopata ili kujikwamua kiuchumi.

Naye Thomasi Maswolwa, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema jitihada za kuwatafutia wananchi wadau wa maendeleo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ambapo pia amesisitiza umuhimu wa kutunza amani na utulivu uliopo nchini ambao umewezesha ushirikiano wa kimataifa kama huu kutoka TIKA.





Wananchi waliopokea msaada huo wamelishukuru shirika la TIKA na Ofisi ya Mbunge kwa kutambua umuhimu wa vikundi vya maendeleo. Walisema msaada huo utasaidia sana vikundi na wanachama mmoja mmoja katika kujikwamua kiuchumi na kuongeza thamani ya mazao yao, hasa mahindi.

No comments:

Post a Comment