Katika sherehe za miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanachama wa CCM kutoka Wilaya ya Songea Vijijini, Jimbo la Madaba, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Thomas Masolwa, wamepongeza na kuunga mkono Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa, uliopitisha azimio la kumteua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa Tanzania Bara, huku Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiteuliwa kugombea urais kwa upande wa Zanzibar.
Akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa
Jimbo la Madaba waliojitokeza kusherehekea miaka 48 ya CCM katika kijiji cha
Lutukila kilichopo kata ya Mkongotema, Masolwa alieleza furaha ya wanachama wa
CCM Jimbo la Madaba kutokana na mafanikio makubwa yaliyofikiwa chini ya uongozi
wa Rais Samia. Ametaja maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu,
kilimo na huduma nyingine za kijamii ambazo zimeboresha maisha ya wananchi, hasa
wa vijijini.
Aidha wanacha hao wamempongeza na kuunga mkono mwenyekiti
wa chama hicho taifa kwa kumchagua Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Katibu
Mkuu wa CCM, kama mgombea mwenza katika uchaguzi ujao.
Masolwa amewataka Wananchi wa Jimbo la Madaba kuendelea
kuiunga mkono CCM kwa kumchagua Rais Samia na viongozi ngazi ya ubunge na
udiwani watakaoteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi ujao
Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Juma
Nambaila, amesema kuwa maadhimisho ya miaka 48 ya CCM yameambatana na shughuli
mbalimbali za kijamii, zilizofanywa na jumuiya za chama ikiwemo upandaji miti,
usafi wa mazingira, na uchangiaji damu,
Mbunge wa Jimbo la Madaba, Dkt. Joseph Mhagama,
ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kutekeleza
miradi ya maendeleo katika jimbo hilo. Amesema wananchi wa Madaba wanapata
manufaa makubwa kutokana na serikali yao kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo
iliyotekelezwa na serikali ya chama cha mapinduzi ikiongozwa na Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan
Sherehe hizi zimeonyesha mshikamano wa wanachama
wa CCM, huku wakiahidi kuendelea kuiunga mkono CCM na Rais Samia katika kipindi
cha uongozi wa Awamu ya Sita.




No comments:
Post a Comment