JALADA LA KESI YA RAIS WA SIMBA SC,AVEVA NA MAKAMU WAKE BADO LIPO KWA DDP.
JALADA la kesi inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Wakili wa Serikali Mkuu, Vitali Peter ameyaeleza hayo kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
Vitalis ameleza kuwa hadi sasa bado wanasubiri kurejeshwa kwa jalada hilo na maelekezo ya kuendelea kama DPP atakuwa amejiridhisha na uchunguzi kuwa umekamilika.
Wakili wa washtakiwa, Evodius Mtawala aliomba ahirisho fupi kwa sababu taratibu za kiofisi haziwezi kuchukua muda mrefu. Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 4,2017.
Evans Elieza Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha USD 300,000.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.
Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.
Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016 Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.
Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.
Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

No comments:
Post a Comment