Pacha walioungana wanafanyiwa kipimo kupitia mashine ya uchunguzi wa
magonjwa ya MRI (Magnetic Resonance Imaging) ambayo itatoa majibu iwapo
wana uwezekano wa kutenganishwa ama la.
Watoto
hao waliozaliwa katika Hospitali ya Misheni ya Berega iliyopo Kanda ya
Mashariki mkoani Morogoro, Julai 21 mwaka huu jana walianza kuchukuliwa
vipimo mbalimbali vya awali.
Akizungumza
na Mwananchi leo Alhamisi Julai 27 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
kwa Umma MNH, Aminiel Aligaesha amesema vipimo bado vinaendelea na
watoto hao wapo chini ya uangalizi maalumu wa madaktari bingwa.
“Jana
walifanyiwa vipimo vya radiolojia kikiwemo cha CT–Scan na leo
watafanyiwa kipimo cha MRI hiki sasa kitatujulisha kuhusu viungo vya
ndani muhimu ikiwemo moyo, figo, ini na vinginevyo,” amesema Aligaesha.
Amesema
majibu ya kipimo hicho yatafanyiwa mashauriano na madaktari bingwa kwa
kushirikiana kwa pamoja ili kuona ni namna gani watawasaidia pacha hao.
“Suala
hili linahitaji mashaurino ya wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya
Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwa kila mtu ana nafasi yake,
tukishakamilisha tutatoa taarifa rasmi iwapo watoto hawa wameungana
sehemu gani nini kitafanyika iwapo inawezekana kuwatenganisha au
haiwezekani,” amesema Aligaesha.
Amefafanua
sababu ya MNH kuwaweka pacha hao chumba cha uangalizi maalumu (ICU)
kuwa ni kutokana na hali waliyonayo hivyo wamewaweka huko ili wasipatwe
na madhara yoyote kiafya,
“Tumewaweka humu ili kuwahudumia na kuwatunza kwa hali ya juu kuhakikisha wanapatiwa huduma zote kwa wakati.” Amesema.
Chanzo Mwananchi

No comments:
Post a Comment