Mkurugenzi
wa Elimu na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard
Kayombo, amewaasa wafanyabiashara nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika
zoezi la ukusanyaji na utoaji wa maoni ya maboresho ya kodi kwa ajili ya
maandalizi ya sharia ya kodi kwa mwaka
mpya wa fedha wa 2025/26.
![]() |
| Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo akizungumza na wafanyabiashara wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma |
Kayombo alitoa wito huu akiwa wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, katika semina iliyohusisha wafanyabiashara, ambapo pia ilifanyika utoaji wa elimu kuhusu mlipa kodi na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara. Katika semina hiyo, Kayombo alisisitiza kuwa serikali kwa sasa ipo katika zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wafanyabiashara ili kuboresha mfumo wa kodi na mazingira ya biashara nchini.
"Serikali inajitahidi kuboresha mazingira ya biashara, na zoezi hili la ukusanyaji maoni ni muhimu ili kubaini changamoto zinazowakabili wafanyabiashara biashara," alisema Kayombo. Aliongeza kuwa, wafanyabiashara wanapaswa kutoa maoni yao kupitia vyombo vya wafanyabiashara na chemba mbalimbali katika maeneo yao ili kusaidia kufikia malengo ya kuboresha mfumo wa kodi na kupunguza malalamiko kutoka kwa jamii ya wafanyabiashara.
![]() |
Aidha, Kayombo alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kulipa kodi kwa hiyari, akieleza kuwa njia hii itasaidia kuongeza mapato ya serikali, hivyo kuweza kuendelea kuwahudumia wananchi kwa huduma bora. "Ikiwa wafanyabiashara wataendelea kulipa kodi kwa hiyari, serikali itaweza kuwekeza katika maendeleo ya jamii na kutoa huduma muhimu," alisisitiza Kayombo.
Semina hii ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na TRA na serikali kwa ujumla kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanapata elimu ya kutosha kuhusu masuala ya kodi na kusaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini.


No comments:
Post a Comment